Friday, November 1, 2013

MANISPAA YA TEMEKE YATENGA ZAIDI YA SHILINGI MILIONI 434 KUIMARISHA USAFI

Halmashauri ya Manispaa ya Temeke yatenga zaidi ya shilingi milioni 434 katika bajeti ya 2013/2014 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya usafi wa mazingira.
Hayo yamesemwa naAfisa Afya Mkuu wa Manispaa ya Temeke  Bw. Ernest Mamuya leo Jijini Dar es salaam wakati wa mkutano na Waandishi wa Habari, Alisema manispaa hiyo imeweza kuendesha ukaguzi  katika maeneo ya kutolea huduma kama hoteli na katika makazi ya watu ili kuwabaini wanaochafua mazingira.
Katika kufanikaisha suala la usafi katika manispaa hiyo vifaa vitakavyonunuliwa ni Compactor 1,tela moja la futi 40 kwa ajili ya usafirishaji taka,ununuzi wa mashine 3 za kusafishia barabara,kununua gari 1 la maji taka na kujenga vizimba 3 vya kuhifadhia taka kwa muda.
Ambapo katika kuhakikisha halmashauri inaongeza kiwango cha udhibiti taka na kuboresha hali ya usafi halmashauri imenunua malori mapya 3 aina ya TATA katika bajeti ya 2012/2013 ambayo yaligharimu milioni 324.
Bw. Mamuya alibainisha kuwa manispaa hiyo ina mikakati mbalimbali ikiwemo  kusafisha maeneo muhimu ikiwa ni pamoja na barabara kuu,maeneo ya wazi, masoko,   mifereji  na kuongeza uwezo wa kukusanya taka,kuzihifadhi na kuzisafirisha kwenda dampo.
Alisema  kuwa Mkakati mwingine ni kuelimisha na kuhamasisha jamii ili iweze kuunga mkono na kushiriki katika kuweka mazingira katika hali ya usafi.
Aliongeza kuwa Halmashauri hiyo imefanikiwa kuzuia magonjwa ya milipuko  kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo kufuatia mikakati kabambe ya kuhamasisha na kusimamia usafi wa Mazingira katika ngazi ya Kaya na kuigawa halmashauri hiyo katika kanda 5 za ufuatiliji na usimamizi wa usafi wa mazingira ili kurahisisha kazi ya ufuatiliaji na usimamizi wa usafi.
Naye Afisa Habari wa Manispaa ya Temeke Lynn Chawala alisema Manispaa hiyo inatarajia kubadili utaratibu wa kutupa taka dampo    la pugu  na kwenda kutupa Kisarawe II  ambapo ni karibu zaidi hali itakayopunguza gharama za kusafirisha taka